Riwaya ya Nguu za Jadi inaanza kwa kumwonyesha Mangwasha na wanawe, Sayore na Kajewa wakiwa wamekimbilia kanisani kutoroka mashambulizi yaliyotekelezwa na Wakule dhidi ya Waketwa. Nje ya jengo hili la kanisa, kunao Waketwa wengine ambao pia walikimbilia pale baada ya makao yao katika eneo la Matango kuchomwa.
Kuna fununu kwamba jamii ya Waketwa inafurushwa kutoka makao yao kwa kuwa kuna watu fulani wanaodhamiria kunyakua ardhi ya Matango kwa nguvu.
Kiongozi wa Matuo, Mtemi Lesulia ambaye ametoka katika jamii ya Wakule anawachukia watu wa jamii ya Waketwa. Wakule na Waketwa wamekuwa na uhasama wa tangu jadi. Kwa upande mwingine, Lonare, kiongozi wa upinzani ana umaarufu mkubwa nchini. Hata hivyo, alitekwa nyara wakati wa uchaguzi, jambo lilimfanya Lesulia kuchaguliwa bila kupingwa.
Katika riwaya hii ya Nguu za Jadi, kuna mhusika kwa jina Mangwasha. Mangwasha ni mwanamke mwenye bidii, na anafanya kazi katika afisi ya Chifu Mshabaha. Chifu huyu ni rafiki mkubwa wa Mtemi Lesulia, naye pia anawachukia Waketwa. Hivyo, anapanga kuwadhulumu Waketwa, jambo ambalo Mangwasha analifahamu kutokana na kufanya kazi naye.
Chifu Mshabaha pia ni rafikiye Sagilu, mzee anayetaka kumuoa Mangwasha licha ya kwamba anajua msichana huyu ana mchumba, Mrima, na wanapanga ndoa. Siku ya harusi ya Mangwasha na Mrima, Sagilu anamtuma kimada wake, Sihaba, akiwa na bomu lililofungwa kama zawadi kwa maharusi. Kwa bahati nzuri, watu wanamshuku na maafa aliyokusudia kufanya hayafanyiki. Sagilu anamnyemelea Mrima na kumzuga kwa kutumia pesa kiasi kwamba Mrima anaisahau familia yake, huku akimwachia Mangwasha jukumu la kuwalea wana wao wawili.
Nchi ya Matuo inakumbwa na matatizo mengi. Kuna matatizoya kiuchumi yanayosababishwa na uongozi mbaya na ufisadi uliokithiri. Mtemi Lesulia anaendeleza ubaguzi dhidi ya Waketwa na vijana wengi walio na elimu hawapati kazi za kujiendeleza kimaisha. Kwa mfano, uteuzi wa wagombea nafasi za uongozi ukiwa umekaribia, machifu wanalazimishwa kuwahamisha Waketwa kutoka Matango ili viongozi wanaopendelewa na mtemi wasipate upinzani, na yeye Mtemi Lesulia asishindwe na mpinzani wake mkuu wa kisiasa, Lonare. Sihaba anatumwa kwenda kuhakikisha kwamba makazi ya Waketwa yameteketezwa,
Anawatumia vijana ambao wanatumia petroli kuchoma makazi hap. Lonare na wafuasi wake wamepeleka kesi mahakamani, na akiwa na wenziwe, kama vile Ngoswe, wanawashawishi watu kurudi katika mako yao ya zamani kule Matango ambako wanajenga mahema. Hata hivyo, siku ya tatu, vijikaratasi vinasambazwa kuwataka watu watoke kwenye ardhi hiyo ambayo, inabainika, imetwaliwa na kupewa Nanzia, mkewe
Mtemi Lesulia, na rafikiye mtemi, Mbwashu. Hawa wanataka kujenga jengo la kibiashara katika ardhi hiyo ya Matango. Watu wanaokuja kuanza ujenzi wanafukuzwa na Waketwa walioamua kuitetea ardhi yao kwa vyovyote vile. Baada ya kuona kwamba mpango wao umetibuka, Mtemi Lesulia anamtumia Sagilu kumpa Mrima pesa nyingi pamoja na ahadi kwamba atapewa kazi serikalini, ilimradi amfanyie Mtemi Lesulia kampeni na kuwaendea kinyume Waketwa.
Kipindi kifupi kabla ya uteuzi wa watakaopeperusha bendera za vyama mbalimbali, Sagilu anatofautiana na mwanawe, Mashauri, baada ya mwanawe kugundua kwamba babake ana
uhusiano wa kimapenzi na mpenzi wake, Cheiya. Mtemi Lesulia naye anakosana na mwanawe, Ngoswe, wakati anapanga njama ya kuvuruga zoezi la uteuzi ili kuwaharibia wapinzani wake nafasi za kuteuliwa. Ngoswe anaona kwamba hatua ya babake inaongozwa na ubinafsi wa kujitakia uongozi na kutojali kwamba baadhi ya watu huenda wakapoteza maisha yao katika vurugu anazopanga. Sagilu anashindwa katika uteuzi na inakuwa wazi kwamba Mtemi Lesulia atakuwa na upinzani mkubwa katika uchaguzi mkuu ujao. Kwa ushawishi wake, Chifu Mshabaha anafutwa kazi na mtemi anaamua kumwondokea Sagilu ambaye sasa anaandamwa na sheria kwa ufisadi alioendesha nchini. Awali, tunaona Mangwasha akipoteza kazi yake katika afisi ya Chifu Mshabaha kwa kujitokeza kama mpinzani wa serikali kwani anamfanyia Lonare kampeni, kando na kwamba mara zote, hakumkubalia Sagilu ombi la kumtaka awe kimada wake. Sihaba anatiwa mbaroni kwa kuendesha biashara haramu ya ukahaba inayosababisha wasichana wengi kuharibika lakini anaachiliwa kutokana na ushawishi aliokuwa nao serikalini. Mikasa hii inawaathiri wahusika wengi vibaya.
Sagilu anapatwa na kichaa na mkewe mtemi, Nanzia, anaugua baada ya jengo lake la kibiashara la Skyline Mall kutwaliwa. Baada ya kulazwa hospitalini kwa muda, anafariki.
Kwa mara nyingine, Lonare anatekwa nyara kabla ya uchaguzi lakini anafaulu kutoroka na kupata matibabu. Uchaguzi mkuu unafanyika na Lonare anachaguliwa kuwa mtemi. Rafikiye Sagilu anashindwa na Mwamba anayechaguliwa kuwa mbunge wa Matango. Lonare anawahutubia wananchi wa Matuo na kuahidi kuufufua uchumi wa nchi na kukabiliana na ufisadi serikalini. Anaahidi pia kwamba serikali yake itashughulikia tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana na kuhakikisha kwamba pana usawa wa kijinsia, akisema kwamba Matuo imesambaratishwa na ubabedume. Anawaomba wananchi wenzake kujiepusha na ukabila na kuwahimiza kukataa na kufichua maovu yanapofanyika nchini. Lonare anachagua kutolipiza kisasi dhidi ya mahasidi wake wa kisiasa.
Kilimani, Nairobi, Kenya
info@kwiksaf.com
+2547974180990
© Kwik Saf. All Rights Reserved. Designed by Kwik Saf Express