Bembea-ya-maisha

Mwongozo wa Bembea Ya Maisha -Maudhui

Maudhui

Katika kazi ya fasihi, maudhui ni mambo muhimu ambayo hujitokeza katika kazi husika. Maswala haya huhusu maisha ya kila siku ya jamii na hujitokeza kupitia matendo na maneno ya wahusika. Katika sehemu hii ya pili ya Mwongozo wa Bembea Ya Maisha tutajaribu kuangazia baadhi ya maudhui yanayojitokeza tamthiliani. Kama hukuwa umesoma sehemu yetu ya kwanza, unaweza kuisoma kwa kubonyeza hapa Mwongozo wa Bembea Ya Maisha.

1. Nafasi ya mwanamke katika jamii

Mwandishi wa Bembea Ya Maisha, Timothy Arege, amefanikiwa kumsawiri mwanamke kama anavyojitokeza katika jamii ya kisasa. Amemwonyesha mwanamke katika njia mbili: chanya na hasi.

 1. Kwanza mwanamke amesawiriwa kama mtu wa kukaa nyumbani na kushughulika na kazi za jikoni. Tunamwona Yona akilalamika kuwa hajaandaliwa chochote cha kula. Sara naye asema kwamba, kila mara yeye hupika, huandaa na kumkaribisha Yona ale. Hapa mwanamke aonekana kuachiwa majukumu ya kupika pale nyumbani.
 2. Kuzaa na kulea kupitia kwa Sara, mwanamke anaonekana kuwa na jukumu la kuwazaa wana na kuwalea. Sara anazaa na kulea Neema, Asna pamoja na Salome. Zaidi ya hayo, anaendelea kuwalea hata katika utu uzima wao.
 3. Mshauri: Sara anawashauri wanawe na hasa Asna kuhusu maswali ya maisha. Anamshauri Asna asimharibie Neema ndoa yake na pia asimchukulie vibaya Bunju. Vile vile anamshauri Neema azungumze na baba yake tena kwa taratibu. Ukurasa wa 69 anamwambia “…Badala ya kumkabili, mshawishi. Atakuelewa…”
 4. Mlaumiwa: Mwanamke aonekana kama mtu wa kulaumiwa haswa kuhusu swala la uzazi. Wanandoa wakikosa kujaliwa watoto, mwanamke analaumiwa; mwana wa kiume akikosekana, wa kulaumiwa ni mwanamke. Sara analaumiwa pale ndoa yao inapochelewa kujaliwa watoto. Lawama haielekezwi kwa Yona> Wanapojaliwa wana wa kike pekee, Sara aelekezewa kidole cha lawama tena na Yona ashauriwa na watu kuoa mwanamke mwingine ili amzalie mwana wa kiume. Kwa haya yote, mwanamke aonekana kupokea lawama toka kwa jamii.
 5. Mvumilivu: Mwanamke amejitokeza pia kama mtu mvumilivu. Sara anavumilia kipigo cha mumewe ambacha kinamwachia maradhi. Anavumilia pia kusemwa na watu kwa kukosa mwana wa kiume.
 6. Mlezi wa Jamii: Tunawaona wanawake katik tamthilia hii wakichorwa kama walezi wa jamii. Sara anailea familia yake wakiwemo wanawe na mumewe. Neema anamshughulikia mama yake (Sara) pamoja na dadazake bila kuisahau familia yake.
 7. Mwanamke awajali wengine: Dina anajitokeza kumsaidia Sara kazi za nyumbani wakati analemewa kutokana na maradhi. Dina anaacha kwake kwenda kumsaidia ilhali Yona anazunguka kwenda kukutana na wenzake badala ya kumsaidia mkewe.
 8. Mlinzi wa desturi ya jamii: Sara anajitokeza kama mtetezi wa desturi za jamii. Anawashauri Neema na Asna kwamba desturi ina mahali pake. Anaunga mkono msimamo wa Bunju kwamba mama mkwe hapaswi kulala kwa mwanawe aliyeolewa.
 9. Chombo cha hekima: Sara anawashauri wanawe kuhusu maswala ya ndoa na unyumba. Anawaambia kuwa mashindano kati ya waume na wake masomoni na kazini ni sawa lakini si nyumbani. Asema kwamba alifunzwa na nyanyake unyagoni kuhusu kila lichotakiwa kufanya. Mafunzo hayo, kwa mujibu wa Sara ndiyo yaliyowafikisha wanawe pale waipo sasa. (UK 67).
 10. Mwanamke vie vile aonekana kutarajiwa kuolewa pindi atimizapo umri wa utu uzima. Sara anamwambis Asna kwamba wakati wao, msichana akibaleghe alikuwa akishinikizwa kuolewa.
 11. Mwanamke aonekana pia kama mtu aliye na bidii maishani. Neema anatia bidii masomoni na hatimaye anafanikiwa na kuweza kuyaendeleza maisha yake na kuwakimu wanuna na wazazi wake.
Advertisement

2. ELIMU

Suala la elimu limepewa kipaumbele katika tamthilia ya Bembea ya Maisha hasa na kizazi cha leo. Maudhui haya yamekuzwa na Yona, Mina, Lemi, Sara na watoto wa Dina.

Yona mwenyewe ameelimika. Kusema kweli, Yona alikuwa mwalimu. Tunamwona akisema kuwa wakati alipokuwa mwalimu, alikuwa akienda skuli wakati wa majira ya alfajiri, kiboko mkononi. Anasema kuwa siku nzima ilikuwa kazi tu, jioni ni darasani tena.

Alipotoka shule, alikuwa akivifunga vitabu kwenye baiskeli kwenda kuvisahihisha wikendi (uk. 62). Yona amesoma hadi Chuo kikuu. Alikuwa mtu wa kwanza pale kijijini kufuzu kutoka chuoni. Mabinti wa Yona na Sara wanasawiriwa kama wasomi.

Elimu ya Neema inadhihirishwa tunapoambiwa kuwa amesoma hadi Chuo kikuu na kuhitimu shahada mbili. Bunju anasema kuwa Asna amesoma hadi Chuo kikuu alikohitimu digrii vilevile. Salome naye ameishi nyumbani kwa Bunju na Neema huku akisoma Shule ya upili. Baadaye anafanikiwa kwenda Chuo kikuu alikopita na kupata first class. Alibahatika kupata ufadhili wa kwenda kuendeleza masomo yake ng’ambo (uk. 28).

Elimu imeonyeshwa kupitia watoto wa Neema na Bunju: Mina na Lemi. Mina anasemekana kuwa anasomea Shule ya bweni. Lemi naye anakuza elimu kwa jinsi anavyoshiriki katika kazi yake ya ziada baada ya kutoka shuleni. Bela anamweleza Neema jinsi Lemi hujinengua anapocheza nyimbo za shuleni. Elimu imesawiriwa kama nguzo ya ufanisi katika maisha ya leo. Wahusika waliosoma na kuhitimu kama vile Yona, Neema na Sara wanafanikiwa kupata kazi na kuwa mwanga wa kijijini.

3. Mabadiliko

Mabadiliko ni hali ya kutoka katika hali moja hadi nyingine. Katika tamthilia hii ya Bembea ya Maisha tunapata kuona mabadiliko kadha:

 • Mabadiliko ya sheria na kanuni za shuleni. Yona anaeleza kuhusu maisha yake ya ujana alipokuwa mwalimu. Alikuwa akirauka alfajiri na mapema kiboko mkononi na mwanafunzi yeyote aliyekuja baada yake angepokea kichapo. Kwa mujibu wa Yona, siku hizi huwezi kumnyooshea mtoto kiboko. Hii ni ithibati ya mabadiliko yaliyoko katika sheria na kanuni zinazomlinda mtoto (wa shule) wa siku hizi. (uk. 62).
 • Mabadiliko kutokana na Sara kudhoofika kiafya. Sara alipoanza kuugua, kuna mengi yaliyobadilika. Yona anaonekana kuhuzunishwa na maradhi ya mke wake. Yona anasema hawezi kuendelea kuishi kama zamani, ni lazima angefuata mkondo mpya wa maisha. Anataka kuzitumia siku zake za uzee kumshughulikia mkewe (uk. 70). Anamwambia Sara pole na kusema kuwa taabu zake Sara zitakuwa taabu zake (uk. 74) S.
 • Mabadiliko ya Yona : Yona amesawiriwa mwanzoni kama mtu mzuri. Lakini baada ya kusutwa na kudharauliwa kwa kukosa mtoto wa kiume anabadilika na kuwa mlevi na kupoteza upendo kwa familia yake. Mapenzi yake kwa mkewe yanageuka na kuwa kichapo. Tunamwona akimpokeza bibiye kichapo cha mbwa hadi kumsababishia maradhi ya moyo. Yona anabadilika kutoka hali hiyo ya ulevi kwa kuamua kuchukuwa mkondo mpya wa maisha (uk. 70). Anasema kwamba pombe imemchezesha kama mwanasesere na kumnyima fursa ya kuilea familia yake.
 • Kuna mabadiliko ya mitazamo ya utamaduni wa jamii ya kizazi cha jana na ya kizazi cha leo. Mabadiliko haya yanajidhihirisha kupitia suala la mtoto wa kike na mtoto wa kiume. Mtazamo wa mtoto wa kike katika kizazi cha jana umebadilishwa na utamaduni wa kizazi cha leo. Kizazi cha jana kinamwona mtoto wa kike kama mtoto asiyekamilika na asiyestahili kusomeshwa wala kurithi mali ya familia (uk. 60). Wazo hili linabadilishwa na kizazi cha leo ambacho kinamwona mtoto wa kike sawa na mtoto wa kiume. Kwa hivyo, kama mtoto wa kiume, yeye pia anaweza kurithi mali ya familia na vilevile kusomeshwa.
 • Mabadiliko ya utamaduni kuhusu ndoa. Kwa mujibu wa Sara, katika maneno yake kwa Asna, wasichana walikuwa wakiozwa punde tu walipobaleghe (uk. 52). Mtindo huu unabadilika miongoni mwa kizazi cha leo kwani wasichana wanaolewa wakati watakapo.
 • Mabadiliko ya utamaduni juu ya mwanaume kuingia jikoni: Yona ambaye, hapo awali, hangeweza kuingia jikoni kumpikia mkewe Sara anabadilika baada ya kugundua kuwa hayo ni mambo yaliyopitwa na wakati. Tunamwona akiandaa kiamshakinywa kwa familia yake. Pia, anamhakikishia Sara kuwa atamshughulikia kwani hali yake Sio nzuri (uk. 62).
 • Kuna mabadiliko ya mitazamo: Kwelekea mwisho wa tamthilia hii, Neema anabadilisha mtazamo wake kuhusu baba yake pale anapompata babaye akiwa amewaandalia kiamshakinyua. (uk. 72). Mwingine anayebadili mtazamo wake ni Bunju. Bunju anabadilisha mtazamo wake wa kutomsaidia Neema kugharamia matibabu ya mamake Sara. Anamwambia anaenda kukutana na mkurugenzi wa kampuni na kuwa akipata hela, atampiga jeki katika suala la matibabu ya mama yake.
 • Mabadiliko ya maisha. Tamthilia hii inaangazia mabadiliko katika maisha ya wanadamu. Kwanza tunapata kuona mabadiliko katika maisha ya Sara. Hali yake ya maisha yabadilika kutoka kuwa ya afya njema na kuwa yenye afya duni. Afya ya Sara inazorota kutokana na ugonjwa wa moyo ambao yaelekea ataishi nao maisha yake yote (uk. 71).
 • Mabadiliko ya mtazamo wa wanajamii kuhusu familia ya Yona. Awali, wanajamii waliidunisha familia ya Yona kwa kukosa mwana wa kiume. Kwa sasa wanaiheshimu familia ya Yona kwa sababu ya mafanikio na elimu ya mabinti wao. Jambo hili linadhihirishwa kupitia maneno ya Luka wakati walikuwa wakiongea na Beni na Yona.

Related Posts

Facebook

Get the Facebook Likebox Slider Pro for WordPress